WAWINDAJI WA HABARI TANZANIA (NEWS HUNTER) Contact Us +255764111)
Disclaimer: The information provided on in this blog is to be used for educational and Entertainment purposes only. The blog author is in no way responsible for any misuse of the information provided.
 photo bcc_zpsbb7aa9b9.jpg Milford Sound in New Zealand

Tuesday, April 30, 2013

Wadau wekezeni katika elimu, asema Mchechu

Singida. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu, amewahimiza wadau wa elimu kuongeza kasi ya kuwekeza kwenye elimu, ili Tanzania iweze kwenda sambamba na mabadiliko makubwa ya kiuchumi na teknolojia yanayoendelea duniani. Mchechu alitoa wito huo juzi alipokuwa akizungumza katika hafla ya kukabidhi msaada wa madawati 260 yenye thamani ya zaidi ya Sh 22 milioni, kwa shule saba za msingi za Wilaya ya Singida. Msaada huo wa madawati umetolewa kwa ushirikiano wa shirika lisilo la kiserikali la Hassan Maajar Trust (HMT) na NHC. Alisemaili nchi yoyote iendelee, inahitaji elimu bora kwa watu wake. “Hivi sasa katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki, tumeungana na nchi jirani katika nyanja za kiuchumi. Hivyo, itoshe tu kusema kuwa hatuwezi kushindana na nchi hizi jirani kama tutapuuzia kuwekeza zaidi kwenye elimu,”alisema Mchechu. Mkurugenzi huyo alisema kuwa pamoja na kulipongeza Shirika la Hassan Maajar Trust kwa uamuzi wake wa kupunguza tatizo la madawati nchini, pia anawasihi wadau wa elimu kuwekeza katika sekta hiyo. “Elimu ndiyo msingi wa kila kitu katika dunia ya sasa, kama alivyotuasa Mwalimu Nyerere, kuwa elimu ni ufunguo wa maisha. Kwa hiyo kuna umuhimu mkubwa wa kuwekeza kwenye sekta ya elimu,”alifafanua Mchechu. Pia alisema Watanzania wanapaswa kujiuliza kuhusu sababu za matokeo mabaya ya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana. Alisema kwa kiwango kikubwa matokeo hayo mabaya yamechangiwa na wazazi/walezi kutokufuatilia maendeleo ya watoto wao ya shule. Mkurugenzi huyo alisema matokeo hayo si tu kwamba ni aibu kwa taifa, lakini yanaonyesha mustakabili mbaya wa elimu kwa taifa. Alisema kwa kuzingatia athari za matokeo kama hayo, kuna haja kwa watu katika ngazi mbalimbali kujiuliza na kubuni mikakati itakayosaidia kuwa hali hiyo haijirudii.
Read More

Monday, April 29, 2013

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika akizungumza wakati Bunge lilipokaa kama kamati kwa ajili ya kupitisha mafungu ya fedha ya Bajeti ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2013/14, mjini Dodoma jana.

Kwa ufupi “Mwaka juzi tulitaka fedha ziongezwe Wizara ya Uchukuzi na Serikali ikasema imeongeza Sh94 bilioni na tukapiga makofi sana hapa, lakini haikuongezwa hata senti moja.” Dodoma. Bajeti ya Wizara ya Maji jana ilipita kwa mbinde baada ya kukwama mara mbili bungeni.Imepita baada ya Serikali kuongeza Sh184.5 bilioni kama Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji ilivyokuwa imependekeza na kuungwa mkono na wabunge wengi. 
Awali, Bajeti hiyo ilikwama kupitishwa tena katika kipindi cha jana asubuhi baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kukatiza mjadala wake kutokana na wabunge kuibana Serikali kwa kukiuka vipengele kadhaa wakati ilipowasilisha upya hoja hiyo. 
Mara ya kwanza Bajeti hiyo ilikwama wiki iliyopita baada ya wabunge kushinikiza kuongezwa kwa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kusambaza maji vijijini. 
Jana asubuhi, Makinda alisitisha shughuli za Bunge saa 5.45 asubuhi ikiwa mapema kabla ya muda wa kawaida wa kumalizika kwa vipindi vya asubuhi ya Bunge ambao ni saa 7.00 mchana baada ya wabunge kupinga utaratibu wa uwasilishaji upya wa Bajeti hiyo. 
Licha ya Serikali kuongeza Sh184.5 bilioni, bado baadhi ya wabunge wa Chadema waliomba Bajeti hiyo iahirishwe kujadiliwa wakisema nyongeza hiyo haina ushahidi wa utekelezaji. 
Baada ya Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa kuwasilisha kauli ya Serikali kuhusu kuongeza fedha kwenye Bajeti ya Wizara ya Maji na Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe kusoma marekebisho ya bajeti yake na kujibu hoja mbalimbali za wabunge, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe alihoji sababu za Serikali kuwasilisha kauli ya kuongeza fedha bila kuwagawia wabunge nakala kama kanuni zinavyotaka. 
“Mwaka juzi tulitaka fedha ziongezwe Wizara ya Uchukuzi na Serikali ikasema imeongeza Sh94 bilioni na tukapiga makofi sana hapa, lakini haikuongezwa hata senti moja.” 
Pia, Zitto alisema mwaka 2011 walikubaliana fedha zinazotokana na ushuru wa mafuta ya taa kupelekwa Wakala wa Umeme Vijijini (Rea), lakini hakuna kilichopelekwa mpaka sasa. 
Kutokana hali hiyo, alitaka hoja hiyo kutolewa kwa maandishi na wabunge wapewe nakala zake ili waibane Serikali pale itakaposhindwa kutekeleza. 
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu ambaye alitinga bungeni baada ya kutumikia adhabu ya kusimamishwa kwa siku tano, alisema kwa mujibu wa taratibu za Bunge, kauli za Serikali lazima zisambazwe kwa wabunge tofauti na kauli ya Waziri wa Fedha akisema hata Spika hakuwa na nakala yoyote huku akisema Waziri alitoa kauli hiyo akiwa hana anachokisoma. 
Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika alitaka hoja hiyo kuondolewa mezani kwa sababu Waziri wa Maji wakati akifanya majumuisho ya hoja yake, hakutoa jedwali linaloonyesha matumizi ya fedha hizo. 
Akitoa mwongozo wake, Spika Makinda alisema Waziri wa Fedha alitoa tamko la Serikali bila wabunge kuwa na nakala kutokana na haraka iliyokuwapo... “Tuliona haiwezekani Waziri wa Maji aseme peke yake juu ya ongezeko la fedha hizo, ndiyo maana Waziri wa Fedha akaja kutoa tamko hapa.” 
Hata hivyo, Makinda alikubaliana na hoja ya Mnyika na kuahirisha Bunge huku akitaka jedwali linaloonyesha matumizi ya fedha hizo liandaliwe.
Read More
Html Free Code