Wadau wekezeni katika elimu, asema Mchechu
Singida. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu, amewahimiza wadau wa elimu kuongeza kasi ya kuwekeza kwenye elimu, ili Tanzania iweze kwenda sambamba na mabadiliko makubwa ya kiuchumi na teknolojia yanayoendelea duniani.
Mchechu alitoa wito huo juzi alipokuwa akizungumza katika hafla ya kukabidhi msaada wa madawati 260 yenye thamani ya zaidi ya Sh 22 milioni, kwa shule saba za msingi za Wilaya ya Singida.
Msaada huo wa madawati umetolewa kwa ushirikiano wa shirika lisilo la kiserikali la Hassan Maajar Trust (HMT) na NHC.
Alisemaili nchi yoyote iendelee, inahitaji elimu bora kwa watu wake.
“Hivi sasa katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki, tumeungana na nchi jirani katika nyanja za kiuchumi. Hivyo, itoshe tu kusema kuwa hatuwezi kushindana na nchi hizi jirani kama tutapuuzia kuwekeza zaidi kwenye elimu,”alisema Mchechu.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa pamoja na kulipongeza Shirika la Hassan Maajar Trust kwa uamuzi wake wa kupunguza tatizo la madawati nchini, pia anawasihi wadau wa elimu kuwekeza katika sekta hiyo.
“Elimu ndiyo msingi wa kila kitu katika dunia ya sasa, kama alivyotuasa Mwalimu Nyerere, kuwa elimu ni ufunguo wa maisha. Kwa hiyo kuna umuhimu mkubwa wa kuwekeza kwenye sekta ya elimu,”alifafanua Mchechu.
Pia alisema Watanzania wanapaswa kujiuliza kuhusu sababu za matokeo mabaya ya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana.
Alisema kwa kiwango kikubwa matokeo hayo mabaya yamechangiwa na wazazi/walezi kutokufuatilia maendeleo ya watoto wao ya shule.
Mkurugenzi huyo alisema matokeo hayo si tu kwamba ni aibu kwa taifa, lakini yanaonyesha mustakabili mbaya wa elimu kwa taifa.
Alisema kwa kuzingatia athari za matokeo kama hayo, kuna haja kwa watu katika ngazi mbalimbali kujiuliza na kubuni mikakati itakayosaidia kuwa hali hiyo haijirudii.

0 comments: